Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraimu
Kwesigabo (kulia) akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai,
2016 ambao umefikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5 za mwezi Juni
2016.Kushoto ni Kaimu Meneja wa wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth Minja.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia
taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Mwezi Julai, 2016 iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraimu Kwesigabo
leo jijini Dar es salaam.
Na Aron Msigwa – Dar es
salaam.
OFISI YA TAIFA YA
TAKWIMU (NBS) imetangaza mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai 2016 na kueleza
kuwa umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5 iliyokuwepo mwezi
Juni mwaka huu.
Akitangaza taarifa ya
mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai, 2016 leo jijini Dar es salaam,
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraimu
Kwesigabo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia
mwezi Julai, 2016 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka
ulioishia mwezi Juni 2016.
Ameeleza kuwa kupungua
kwa mfumuko wa Bei wa mwezi Julai 2016 kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya bei
ya baadhi ya bidhaa za vyakula na zile zisizo za vyakula kwa kipindi
kilichoishia Julai 2016 zikiwemo bidhaa za samaki kwa asilimia 6.6, mafuta ya
kupikia asilimia 4.9 na maharage kwa asilimia 1.9 huku bei zisizo za vyakula
zikihusisha ni gesi kwa asilimia 21.5,
mafuta ya taa 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3.
Kwa upande wa bidhaa zisizo
za vyakula zilizoonesha kupungua bei ni pamoja na bidhaa za gesi kwa asilimia
21.5, mafuta ya taa kwa asilimia 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3.
Aidha, ameeleza kuwa
pamoja kupungua huko, kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia
mwezi Julai, 2016 kwenye baadhi ya bidhaa umeonesha kuongezeka katika kipindi
hicho hasa kwenye kama mchele, mahindi,
unga wa mahindi, vyakula kwenye migahawa na mkaa.
Bw. Kwesigabo amesema
kuwa Fahirisi za Bei nazo zimeongezeka hadi kufikia 103.50 mwezi Julai, 2016 kutoka
103.47 za mwezi Juni 2016, ongezeko ambalo
limechangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula zile zisizokuwa za vyakula.
Amesema ongezeko hilo
la Fahirisi linahusisha kundi la bidhaa na huduma za vyakula na vinywaji
baridi, Vinywaji vyenye kilevi na bidhaa za Tumbaku, Mavazi ya nguo na viatu,
nishati, maji na Makazi pamoja na Samani, vifaa vya nyumbani na ukarabati wa
nyumba.
Kundi lingine linahusisha
gharama za Afya, usafirishaji, Mawasiliano, Utamaduni na Burudani, Elimu,
hoteli na migahawa pamoja na bidhaa na huduma nyinginezo ambazo jumla ya
Fahirisi za Bidhaa hizo kwa mwezi huo zimefikia 103.50.
“Baadhi ya bidhaa
zilizo sababisha kuongezeka kwa Fahirisi ni pamoja na mafuta ya kupikia asilimia
1.1, samaki wabichi asilimia 6.0, matunda asilimia 4.9, maharage makavu kwa
asilimia 2.7, ndizi za kupika asilimia 1.9 na mahindi kwa asilimia 1.5”
Amesisitiza Kwesigabo.
Mbali na hilo ameeleza kuwa
Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai 2016
umepungua hadi kufikia asilimia 7.6 kutoka asilimia 8.1 ya mwezi Juni 2016.
Kwa upande wa uwezo wa shilingi
ya 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia shilingi 96 na
senti 62 mwezi Julai 2016 ikilinganishwa na shilingi 96 na senti 65 ya mwezi
Juni, 2016.
Aidha, hali ya Mfumuko
wa Bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki imeonesha kuwa nchi ya Kenya
Mfumuko wa Bei wa mwezi Julai umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.39 kutoka
asilimia 5.80 za mwezi Juni, 2016, Uganda ikiwa na Mfumuko wa Bei uliopungua wa
asilimia 5.1 kwa mwezi Julai kutoka asilimia 5.9 za mwezi Juni, 2016.